← Isaiah (26/66) → |
1. | Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma. |
2. | Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie. |
3. | Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. |
4. | Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele. |
5. | Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini. |
6. | Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji. |
7. | Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. |
8. | Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee Bwana; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako. |
9. | Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki. |
10. | Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa Bwana. |
11. | Bwana, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako. |
12. | Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. |
13. | Ee Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako. |
14. | Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajilia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao. |
15. | Umeliongeza hilo taifa, Bwana, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii. |
16. | Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. |
17. | Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee Bwana. |
18. | Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. |
19. | Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa. |
20. | Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita. |
21. | Kwa maana, tazama, Bwana anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa. |
← Isaiah (26/66) → |