← Isaiah (24/66) → |
1. | Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake. |
2. | Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida. |
3. | Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana Bwana amenena neno hilo. |
4. | Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. |
5. | Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. |
6. | Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu. |
7. | Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua. |
8. | Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma. |
9. | Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao. |
10. | Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote. |
11. | Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka. |
12. | Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu. |
13. | Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake. |
14. | Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa Bwana watapiga kelele toka baharini. |
15. | Basi, mtukuzeni Bwana katika mashariki, litukuzeni jina la Bwana, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. |
16. | Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. |
17. | Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. |
18. | Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. |
19. | Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. |
20. | Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena. |
21. | Tena itakuwa katika siku hiyo, Bwana ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; |
22. | nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa. |
23. | Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa Bwana wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu. |
← Isaiah (24/66) → |