← Isaiah (23/66) → |
1. | Ufunuo juu ya Tiro. Toeni sauti za uchungu, enyi merikebu za Tarshishi, kwa maana umeharibika kabisa, hata hapana nyumba, hapana mahali pa kuingia; toka nchi ya Kitimu wamefunuliwa habari. |
2. | Tulieni, enyi mkaao kisiwani; wewe ambaye wafanya biashara wa Sidoni, wavukao bahari, walikujaza. |
3. | Vitu vilivyopandwa, vya Shihori, mavuno ya Nile, yaliyokuja juu ya maji mengi, ndiyo pato lake, naye alikuwa soko la mataifa. |
4. | Tahayari, Ee Sidoni; kwa maana bahari imenena, hiyo ngome ya bahari ilisema, Sikuona utungu, wala sikuzaa, wala sikulea vijana, wala sikulea wanawali. |
5. | Habari itakapofika Misri wataona uchungu sana kwa sababu ya habari ya Tiro. |
6. | Piteni mpaka Tarshishi, enyi mkaao kisiwani, toeni sauti ya uchungu. |
7. | Je! Huu ndio mji wenu wa furaha, ambao mwanzo wake ulikuwako tangu siku za kale, ambao miguu yake ilimchukua akae mbali sana? |
8. | Ni nani aliyefanya shauri hili juu ya Tiro, uliotia watu taji, ambao wafanya biashara wake walikuwa wana wa wafalme, na wachuuzi wake ni watu wakuu wa dunia? |
9. | Bwana wa majeshi ndiye aliyefanya shauri hili, ili kuharibu kiburi cha utukufu wote, na kuwaaibisha watu wa duniani wote pia. |
10. | Pita katika nchi yako, kama Nile, Ee binti wa Tarshishi, hapana tena mshipi wa kukuzuia. |
11. | Amenyosha mkono wake juu ya bahari, amezitikisa falme; Bwana ametoa amri katika habari za Kanaani, kuziangamiza ngome zake. |
12. | Naye akasema, Usizidi kufurahi, ewe bikira uliyeaibishwa, binti wa Sidoni, haya, ondoka, uende hata Kitimu; huko nako hutapata raha. |
13. | Tazama, nchi ya Wakaldayo; watu hao hawako tena; Mwashuri ameiweka tayari kwa hayawani wa jangwani; wamesimamisha buruji zao za vita, wameyaharibu majumba yake ya enzi, akaufanya kuwa uharibifu. |
14. | Pigeni yowe, enyi merikebu za Tarshishi; maana ngome yenu imefanywa ukiwa. |
15. | Basi, itakuwa katika siku ile, Tiro utasahauliwa miaka sabini, kadiri ya siku za mfalme mmoja; hata mwisho wa miaka sabini, Tiro utakuwa kama vile ulivyo wimbo wa kahaba. |
16. | Twaa kinubi, tembea mjini, Ewe kahaba uliyesahauliwa; Piga vizuri, imba nyimbo nyingi, Upate kukumbukwa tena. |
17. | Hata itakuwa mwisho wa miaka sabini, Bwana ataizuru nchi ya Tiro, naye atarudi apate ujira wake, atafanya ukahaba pamoja na falme zote za ulimwengu juu ya uso wa dunia. |
18. | Na biashara yake na ujira wake utakuwa wakfu kwa Bwana, hautawekwa hazinani wala hautawekwa akiba; bali mapato ya biashara yake yatakuwa mali zao wakaao mbele za Bwana, wapate kula na kushiba, na kuvaa mavazi ya fahari. |
← Isaiah (23/66) → |