| ← Isaiah (19/66) → | 
| 1. | Ufunuo juu ya Misri. Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake. | 
| 2. | Nami nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme. | 
| 3. | Na roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli, na kwa wachawi. | 
| 4. | Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, Bwana wa majeshi. | 
| 5. | Na maji ya baharini yatapunguka, na huo mto utakauka na kuwa pakavu. | 
| 6. | Na vijito vya mto vitatoa uvundo, na mifereji ya Misri itakuwa haina maji mengi, itakauka; manyasi na mianzi itanyauka. | 
| 7. | Vitu vimeavyo karibu na Nile, katika ukingo wa Nile, na vyote vilivyopandwa karibu na Nile vitakauka na kuondolewa na kutoweka. | 
| 8. | Na wavuvi wataugua, na wote wavuao kwa ndoana watahuzunika, nao watandao jarife juu ya maji watazimia. | 
| 9. | Tena wao wafanyao kazi ya kuchana kitani watafadhaika, na hao pia wafumao bafta. | 
| 10. | Na nguzo za nchi zitavunjika vipande vipande, wote wafanyao kazi ya mshahara watahuzunika nafsini mwao. | 
| 11. | Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, shauri lao limepumbazika; mwawezaje kumwambia Farao, Mimi ni mwana wa wenye hekima, ni mwana wa wafalme wa zamani? | 
| 12. | Wako wapi, basi, watu wako wenye hekima? Na wakuambie sasa; na wajue mambo aliyokusudia Bwana wa majeshi juu ya Misri. | 
| 13. | Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu, wakuu wa Nofu wamedanganyika; na hao walio mawe ya pembeni ya kabila zake wameikosesha Misri. | 
| 14. | Yeye Bwana ametia roho ya ushupavu katika moyo wa Misri, nao wameikosesha Misri katika matendo yake yote, kama mlevi aendavyo huko na huko akitapika. | 
| 15. | Wala haitakuwako kazi yo yote katika Misri iwezayo kufanywa, ya kichwa au ya mkia, ya tawi au ya nyasi. | 
| 16. | Katika siku hiyo Misri itakuwa kama wanawake; itatetemeka na kuogopa kwa sababu ya kutikiswa kwa mkono wa Bwana wa majeshi, autikisao juu yake. | 
| 17. | Na nchi ya Yuda itakuwa sababu ya utisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi la Bwana wa majeshi, analolikusudia juu yake. | 
| 18. | Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia Bwana wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu. | 
| 19. | Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa Bwana, na nguzo mpakani mwake kwa Bwana. | 
| 20. | Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa. | 
| 21. | Na Bwana atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua Bwana katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea Bwana nadhiri, na kuzitekeleza. | 
| 22. | Naye Bwana atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa Bwana, atakubali maombi yao na kuwaponya. | 
| 23. | Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri. | 
| 24. | Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia; | 
| 25. | kwa kuwa Bwana wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu. | 
| ← Isaiah (19/66) → |