Isaiah (15/66)  

1. Ufunuo juu ya Moabu. Maana katika usiku mmoja Ari wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa; maana katika usiku mmoja Kiri wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa.
2. Wanapanda juu hata Bayithi na Diboni, mpaka mahali palipo juu ili walie; juu ya Nebo na juu ya Medeba Wamoabi wanalia; Wana upaa juu ya vichwa vyao vyote; kila ndevu zimenyolewa.
3. Wanajivika nguo za magunia katika njia kuu zao; juu ya dari zao, na katika mitaa yao, kila mtu analia, anamwaga machozi.
4. Heshboni analia na Eleale; mpaka Yahasa sauti ya kulia kwao inasikiwa; hata watu wa Moabu waliovaa silaha wanapiga kelele sana kwa sababu hiyo; nafsi yake inatetemeka ndani yake.
5. Moyo wangu unamlilia Moabu; wakuu wake wanakimbilia Soari kama ndama wa miaka mitatu; kwa maana wanapanda mbavu za Luhithi wakilia; maana katika njia iendayo hata Horonaimu wanapaliza sauti ya kukata tamaa.
6. Kwa maana maji ya Nimrimu yamekuwa mahali palipoharibika, kwa kuwa majani yamekauka, miche imenyauka, majani mabichi yamekoma.
7. Kwa hiyo vitu walivyojipatia tele, na akiba yao, wanavichukua hata kijito cha mierebi.
8. Maana kilio hicho kimezunguka mipaka ya Moabu, malalamiko yao yamefika hata Eglaimu, na malalamiko yao hata Beer-Elimu.
9. Maana maji ya Dimoni yamejaa damu; maana ninaweka tayari msiba mpya juu ya Dimoni, simba juu ya watu wa Moabu waliokimbia, na juu ya mabaki yao.

  Isaiah (15/66)