| ← Isaiah (14/66) → | 
| 1. | Maana Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo. | 
| 2. | Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea. | 
| 3. | Tena itakuwa katika siku ile, ambayo Bwana atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa; | 
| 4. | utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri! | 
| 5. | Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala. | 
| 6. | Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu. | 
| 7. | Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata huanzilisha kuimba. | 
| 8. | Naam, misunobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia. | 
| 9. | Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi. | 
| 10. | Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! | 
| 11. | Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika. | 
| 12. | Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! | 
| 13. | Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. | 
| 14. | Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. | 
| 15. | Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo. | 
| 16. | Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme; | 
| 17. | Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? | 
| 18. | Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe; | 
| 19. | Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa; Kama vazi la wale waliouawa, Wale waliochomwa kwa upanga, Wale washukao mpaka misingi ya shimo; Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu. | 
| 20. | Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako; Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele. | 
| 21. | Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, Na kuujaza miji uso wa ulimwengu. | 
| 22. | Nami nitainuka, nishindane nao; asema Bwana wa majeshi; na katika Babeli nitang'oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema Bwana. | 
| 23. | Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema Bwana wa majeshi. | 
| 24. | Bwana wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea; | 
| 25. | kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao. | 
| 26. | Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. | 
| 27. | Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma? | 
| 28. | Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi. | 
| 29. | Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, Kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; Maana katika shina la nyoka atatoka fira, Na uzao wake ni joka la moto arukaye | 
| 30. | Nao walio maskini kabisa watakula, Na wahitaji watajilaza salama; Nami nitatia shina lako kwa njaa, Na mabaki yako watauawa. | 
| 31. | Piga yowe, Ee lango; lia, Ee mji; Ee Ufilisti, pia wote, umeyeyuka kabisa; Maana moshi unakuja toka kaskazini, Wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake. | 
| 32. | Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani? Ya kuwa Bwana ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio. | 
| ← Isaiah (14/66) → |