← Isaiah (13/66) → |
1. | Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi. |
2. | Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu. |
3. | Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari. |
4. | Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; Bwana wa majeshi anapanga jeshi kwa vita; |
5. | watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, Bwana na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote. |
6. | Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. |
7. | Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. |
8. | Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto. |
9. | Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. |
10. | Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. |
11. | Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali; |
12. | nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri. |
13. | Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. |
14. | Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe. |
15. | Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. |
16. | Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri. |
17. | Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. |
18. | Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. |
19. | Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. |
20. | Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. |
21. | Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. |
22. | Na mbwa-mwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka. |
← Isaiah (13/66) → |