Isaiah (11/66)  

1. Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
2. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;
3. na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;
4. bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.
5. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.
6. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7. Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.
10. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.
11. Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari.
12. Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.
13. Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu.
14. Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.
15. Na Bwana atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu.
16. Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.

  Isaiah (11/66)