← Isaiah (10/66) → |
1. | Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; |
2. | ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang'anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! |
3. | Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? |
4. | Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. |
5. | Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! |
6. | Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. |
7. | Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. |
8. | Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme? |
9. | Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski? |
10. | Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria; |
11. | je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake? |
12. | Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake. |
13. | Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. |
14. | Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. |
15. | Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. |
16. | Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. |
17. | Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja. |
18. | Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa. |
19. | Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu. |
20. | Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea Bwana, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli. |
21. | Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu. |
22. | Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki. |
23. | Kwa maana Bwana, Bwana wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote. |
24. | Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri. |
25. | Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza. |
26. | Na Bwana wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri. |
27. | Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta. |
28. | Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi; |
29. | wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia. |
30. | Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi! |
31. | Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie; |
32. | siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu. |
33. | Angalia, Bwana, Bwana wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini; |
34. | naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza. |
← Isaiah (10/66) → |