Isaiah (1/66) → |
1. | Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. |
2. | Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. |
3. | Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. |
4. | Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. |
5. | Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. |
6. | Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta. |
7. | Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni. |
8. | Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa. |
9. | Kama Bwana wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora. |
10. | Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. |
11. | Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. |
12. | Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? |
13. | Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. |
14. | Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. |
15. | Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. |
16. | Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; |
17. | jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. |
18. | Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. |
19. | Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; |
20. | bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya. |
21. | Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji! |
22. | Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji. |
23. | Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii. |
24. | Kwa hiyo, asema Bwana, Bwana wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitatwaa kisasi kwa adui zangu; |
25. | nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote; |
26. | nami nitarejeza upya waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu. |
27. | Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki. |
28. | Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao Bwana watateketezwa. |
29. | Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua. |
30. | Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji. |
31. | Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima. |
Isaiah (1/66) → |