| ← Hosea (8/14) → |
| 1. | Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya Bwana; kwa sababu wamelihalifu agano langu, wameiasi sheria yangu. |
| 2. | Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua. |
| 3. | Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia. |
| 4. | Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. |
| 5. | Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? |
| 6. | Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. |
| 7. | Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. |
| 8. | Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza. |
| 9. | Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa mwituni aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi. |
| 10. | Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu. |
| 11. | Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. |
| 12. | Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. |
| 13. | Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri. |
| 14. | Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitapeleka moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake. |
| ← Hosea (8/14) → |