Hosea (7/14)  

1. Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang'anyi hushambulia nje.
2. Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.
3. Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.
4. Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu.
5. Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.
6. Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.
7. Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
8. Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.
9. Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari.
10. Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia Bwana, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.
11. Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.
12. Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.
13. Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.
14. Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.
15. Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.
16. Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.

  Hosea (7/14)