| ← Hosea (4/14) → |
| 1. | Lisikieni neno la Bwana, enyi wana wa Israeli; kwa maana Bwana ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. |
| 2. | Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu. |
| 3. | Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa. |
| 4. | Walakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani. |
| 5. | Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako. |
| 6. | Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako. |
| 7. | Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. |
| 8. | Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao. |
| 9. | Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao. |
| 10. | Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia Bwana. |
| 11. | Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. |
| 12. | Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao. |
| 13. | Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. |
| 14. | Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia. |
| 15. | Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo Bwana. |
| 16. | Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! Bwana atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi! |
| 17. | Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. |
| 18. | Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. |
| 19. | Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao. |
| ← Hosea (4/14) → |