Hosea (13/14)  

1. Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa.
2. Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyizia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama.
3. Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba.
4. Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna Mwokozi.
5. Mimi nalikujua katika jangwa, katika nchi yenye kiu nyingi.
6. Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi.
7. Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani;
8. nitakutana nao kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua.
9. Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, ya kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako.
10. Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu?
11. Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu.
12. Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba.
13. Utungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto.
14. Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu.
15. Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya Bwana itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo.
16. Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatambuliwa.

  Hosea (13/14)