Hosea (1/14)  

1. Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.
2. Hapo kwanza Bwana aliponena kwa kinywa cha Hosea, Bwana alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha Bwana.
3. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume.
4. Bwana akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli.
5. Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
6. Akachukua mimba tena, akazaa mtoto mwanamke. Bwana akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama
7. Lakini nitairehemu nyumba ya Yuda; nitawaokoa kwa Bwana, Mungu wao; wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa silaha, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi.
8. Basi, akiisha kumwachisha Lo-ruhama, akachukua mimba, akazaa mtoto mwanamume.
9. Bwana akasema, Mwite jina lake Lo-ami
10. Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.
11. Na wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanyika pamoja, nao watajiwekea kichwa kimoja, nao watakwea watoke katika nchi hii; kwa maana siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.

      Hosea (1/14)