Haggai (1/2)  

1. Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema,
2. Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana.
3. Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,
4. Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?
5. Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
6. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.
7. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
8. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.
9. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema Bwana wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.
10. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.
11. Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.
12. Ndipo Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, pamoja na hayo mabaki yote ya watu, wakaitii sauti ya Bwana, Mungu wao, na maneno ya Hagai nabii, kama Bwana, Mungu wao, alivyomtuma; nao watu wakaogopa mbele za Bwana.
13. Ndipo Hagai mjumbe wa Bwana, katika ujumbe wa Bwana, akawaambia watu, akisema, Mimi nipo pamoja nanyi, asema Bwana.
14. Bwana akaiamsha roho ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na roho ya Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na roho zao mabaki ya watu; wakaenda, wakafanya kazi katika nyumba ya Bwana wa majeshi, Mungu wao;
15. katika siku ya ishirini na nne ya mwezi, katika mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa Dario mfalme.

      Haggai (1/2)