← Habakkuk (2/3) → |
1. | Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. |
2. | Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. |
3. | Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. |
4. | Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake. |
5. | Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu. |
6. | Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani! |
7. | Je! Hawatainuka ghafula wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao? |
8. | Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. |
9. | Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu! |
10. | Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako. |
11. | Kwa maana jiwe litapiga kelele katika ukuta, nayo boriti katika miti italijibu. |
12. | Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu! |
13. | Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa Bwana wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili? |
14. | Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari. |
15. | Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao! |
16. | Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kuume wa Bwana kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako. |
17. | Kwa maana udhalimu uliotendwa juu ya Lebanoni utakufunikiza, na kuangamizwa kwao wanyama kutakutia hofu; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake. |
18. | Sanamu ya kuchora yafaa nini, hata yeye aliyeifanya ameichora? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema? |
19. | Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa. |
20. | Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake. |
← Habakkuk (2/3) → |