← Genesis (49/50) → |
1. | Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. |
2. | Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu. |
3. | Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. |
4. | Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu. |
5. | Simeoni na Lawi ni ndugu; Panga zao ni silaha za jeuri. |
6. | Nafsi yangu, usiingie katika siri yao, Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao, Maana katika ghadhabu yao walimuua mtu, Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe; |
7. | Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli. |
8. | Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. |
9. | Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha? |
10. | Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii. |
11. | Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwana-punda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu. |
12. | Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa. |
13. | Zabuloni atakaa pwani ya bahari, Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu, Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni. |
14. | Isakari ni punda hodari, Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo; |
15. | Akaona mahali pa raha, kuwa pema, Na nchi, ya kuwa ni nzuri, Akainama bega lake lichukue mizigo, Akawa mtumishi kwa kazi ngumu. |
16. | Dani atahukumu watu wake, Kama moja ya makabila ya Israeli; |
17. | Dani atakuwa nyoka barabarani, Bafe katika njia, Aumaye visigino vya farasi, Hata apandaye ataanguka chali. |
18. | Wokovu wako nimeungoja, Ee Bwana. |
19. | Gadi, jeshi litamsonga, Lakini atawasonga wao mpaka visigino. |
20. | Asheri, chakula chake kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme. |
21. | Naftali ni ayala aliyefunguliwa; Anatoa maneno mazuri. |
22. | Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matwi yake yametanda ukutani. |
23. | Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, |
24. | Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli, |
25. | Naam, kwa Mungu wa baba yako atakaye kusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba. |
26. | Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake. |
27. | Benyamini ni mbwa-mwitu mwenye kurarua-rarua Asubuhi atakula mawindo, Na jioni atagawanya mateka. |
28. | Hizo zote ndizo kabila za Israeli kumi na mbili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa mbaraka wake aliwabariki. |
29. | Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; |
30. | katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia. |
31. | Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea; |
32. | shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi. |
33. | Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake. |
← Genesis (49/50) → |