← Genesis (47/50) → |
1. | Ndipo Yusufu akaja akamwarifu Farao, akasema, Baba yangu, na ndugu zangu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo, wamekuja kutoka nchi ya Kanaani, nao wako katika nchi ya Gosheni. |
2. | Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao. |
3. | Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu. |
4. | Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni. |
5. | Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia; |
6. | nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu. |
7. | Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao. |
8. | Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? |
9. | Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao. |
10. | Yakobo akambariki Farao, akatoka mbele ya Farao. |
11. | Yusufu akawakalisha babaye na nduguze, na kuwapa milki katika nchi ya Misri, katika mahali pazuri pa nchi, katika nchi ya Ramesesi, kama Farao alivyoamuru. |
12. | Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao. |
13. | Wala hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, hata nchi ya Misri, na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa. |
14. | Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. |
15. | Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. |
16. | Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. |
17. | Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng'ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. |
18. | Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. |
19. | Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee. |
20. | Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. |
21. | Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. |
22. | Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao. |
23. | Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi. |
24. | Itakuwa wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu. |
25. | Wakasema, Umetulinda hai, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao. |
26. | Yusufu akaifanya sheria kwa habari ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao. |
27. | Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana. |
28. | Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi siku za miaka ya maisha yake Yakobo ilikuwa miaka mia moja na arobaini na saba. |
29. | Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri. |
30. | Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema. |
31. | Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda. |
← Genesis (47/50) → |