← Genesis (45/50) → |
1. | Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. |
2. | Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. |
3. | Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. |
4. | Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. |
5. | Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. |
6. | Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. |
7. | Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. |
8. | Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. |
9. | Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. |
10. | Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng'ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko; |
11. | maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo. |
12. | Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. |
13. | Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu. |
14. | Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake. |
15. | Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye |
16. | Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake. |
17. | Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; |
18. | kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. |
19. | Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. |
20. | Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. |
21. | Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. |
22. | Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. |
23. | Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. |
24. | Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani. |
25. | Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao. |
26. | Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. |
27. | Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. |
28. | Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa. |
← Genesis (45/50) → |