← Genesis (44/50) → |
1. | Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. |
2. | Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. |
3. | Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao. |
4. | Na walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema? |
5. | Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi. |
6. | Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo. |
7. | Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? |
8. | Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi; tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu, tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa bwana wako fedha au dhahabu? |
9. | Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu. |
10. | Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia. |
11. | Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake. |
12. | Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini. |
13. | Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini. |
14. | Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi. |
15. | Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi? |
16. | Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake. |
17. | Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi enendeni zenu kwa amani kwa baba yenu. |
18. | Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. |
19. | Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu? |
20. | Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. |
21. | Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. |
22. | Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa. |
23. | Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena |
24. | Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. |
25. | Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. |
26. | Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. |
27. | Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili; |
28. | mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. |
29. | Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. |
30. | Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana; |
31. | itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini. |
32. | Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu sikuzote. |
33. | Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze. |
34. | Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu. |
← Genesis (44/50) → |