← Genesis (42/50) → |
1. | Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana? |
2. | Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife. |
3. | Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka. |
4. | Walakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate. |
5. | Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. |
6. | Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. |
7. | Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula. |
8. | Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye. |
9. | Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi. |
10. | Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula. |
11. | Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi. |
12. | Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi. |
13. | Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko. |
14. | Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi. |
15. | Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo. |
16. | Mpelekeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa, hata maneno yenu yahakikishwe, kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao, ninyi ni wapelelezi. |
17. | Akawatia wote gerezani siku tatu. |
18. | Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. |
19. | Kama ni wa kweli ninyi ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, |
20. | mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. |
21. | Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata. |
22. | Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. |
23. | Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. |
24. | Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao. |
25. | Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. |
26. | Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko. |
27. | Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake. |
28. | Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N'nini hii Mungu aliyotutendea? |
29. | Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema, |
30. | Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi. |
31. | Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi. |
32. | Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani. |
33. | Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu. |
34. | Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii. |
35. | Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa. |
36. | Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi. |
37. | Reubeni akamwambia babaye, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako. |
38. | Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini. |
← Genesis (42/50) → |