← Genesis (41/50) → |
1. | Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. |
2. | Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. |
3. | Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. |
4. | Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. |
5. | Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. |
6. | Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. |
7. | Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. |
8. | Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. |
9. | Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. |
10. | Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. |
11. | Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. |
12. | Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. |
13. | Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. |
14. | Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. |
15. | Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. |
16. | Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. |
17. | Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto; |
18. | na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini. |
19. | Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. |
20. | Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. |
21. | Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. |
22. | Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. |
23. | Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. |
24. | Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake. |
25. | Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. |
26. | Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. |
27. | Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. |
28. | Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. |
29. | Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. |
30. | Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. |
31. | Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. |
32. | Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. |
33. | Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. |
34. | Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. |
35. | Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. |
36. | Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. |
37. | Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. |
38. | Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? |
39. | Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. |
40. | Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. |
41. | Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. |
42. | Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. |
43. | Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. |
44. | Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. |
45. | Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri. |
46. | Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri. |
47. | Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi. |
48. | Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake. |
49. | Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu. |
50. | Kabla ya kuja miaka ya njaa, Yusufu akazaliwa wana wawili, ambao Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia. |
51. | Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu. |
52. | Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu. |
53. | Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri, |
54. | ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula. |
55. | Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. |
56. | Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. |
57. | Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote. |
← Genesis (41/50) → |