← Genesis (4/50) → |
1. | Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. |
2. | Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. |
3. | Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. |
4. | Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; |
5. | bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. |
6. | Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? |
7. | Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. |
8. | Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. |
9. | Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? |
10. | Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. |
11. | Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; |
12. | utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. |
13. | Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. |
14. | Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. |
15. | Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. |
16. | Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni. |
17. | Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe. |
18. | Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki. |
19. | Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. |
20. | Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. |
21. | Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. |
22. | Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama. |
23. | Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua; |
24. | Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba. |
25. | Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua. |
26. | Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana. |
← Genesis (4/50) → |