← Genesis (37/50) → |
1. | Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. |
2. | Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. |
3. | Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. |
4. | Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. |
5. | Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; |
6. | akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. |
7. | Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. |
8. | Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. |
9. | Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. |
10. | Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? |
11. | Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. |
12. | Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. |
13. | Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. |
14. | Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. |
15. | Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? |
16. | Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. |
17. | Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. |
18. | Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. |
19. | Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. |
20. | Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. |
21. | Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. |
22. | Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. |
23. | Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, |
24. | wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. |
25. | Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. |
26. | Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? |
27. | Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. |
28. | Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. |
29. | Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. |
30. | Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? |
31. | Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. |
32. | Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. |
33. | Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. |
34. | Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. |
35. | Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia. |
36. | Nao Wamidiani wakamwuza huko Misri, kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari. |
← Genesis (37/50) → |