| ← Genesis (34/50) → |
| 1. | Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. |
| 2. | Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. |
| 3. | Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. |
| 4. | Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. |
| 5. | Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja. |
| 6. | Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. |
| 7. | Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka. |
| 8. | Hamori akasema nao, akinena, Roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. |
| 9. | Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. |
| 10. | Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. |
| 11. | Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. |
| 12. | Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. |
| 13. | Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, umbu lao, |
| 14. | wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe umbu letu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. |
| 15. | Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, |
| 16. | ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. |
| 17. | Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa umbu letu, nasi tutakwenda zetu. |
| 18. | Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. |
| 19. | Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye. |
| 20. | Hamori, na Shekemu mwanawe, wakaja langoni pa mji wao, wakasema na watu wa mji wao, wakinena, |
| 21. | Watu hawa wana amani nasi, basi na wakae katika nchi, na kufanya biashara humo; kwa maana nchi ni kubwa, yawatosha; na tuwatwae binti zao kuwa wake zetu, na binti zetu tuwape wao. |
| 22. | Lakini kwa sharti hiyo moja tu watapatana nasi wakae wote kwetu, tuwe watu wamoja, kama tukitahiriwa kila mwanamume, kama hawa walivyotahiriwa. |
| 23. | Je! Kondoo zao, na mali zao, na wanyama wao wote hawatakuwa mali zetu? Basi na tupatane nao tu, nao watakaa kwetu. |
| 24. | Wakawasikia Hamori na Shekemu mwanawe, wote watokao katika lango la mji wake. Wakatahiriwa kila mwanamume, wote watokao katika lango la mji wake. |
| 25. | Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wakiumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, nduguze Dina, wakatwaa kila mtu upanga wake, wakaujia mji kwa ujasiri, wakawaua waume wote. |
| 26. | Wakawaua Hamori, na Shekemu mwanawe, kwa makali ya upanga, wakamtwaa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakatoka. |
| 27. | Wana wa Yakobo wakawajilia hao waliouawa, wakauteka nyara mji kwa sababu wamemharibu umbu lao. |
| 28. | Wakachukua kondoo zao, na ng'ombe zao, na punda zao, na vitu vilivyokuwamo mjini, navyo vilivyokuwako kondeni. |
| 29. | Wakatwaa na mali zao zote, na watoto wao wote, na wake zao, na vyote vilivyokuwamo nyumbani mwao wakavichukua mateka. |
| 30. | Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, Mmenitaabisha, kunifanya ninuke vibaya kati ya watu wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi; na mimi, kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu. |
| 31. | Nao wakasema, Je! Ni vema amtendee umbu letu kama kahaba? |
| ← Genesis (34/50) → |