← Genesis (33/50) → |
1. | Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao. |
2. | Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho. |
3. | Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. |
4. | Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. |
5. | Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. |
6. | Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. |
7. | Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. |
8. | Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. |
9. | Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. |
10. | Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. |
11. | Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea. |
12. | Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia. |
13. | Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. |
14. | Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri. |
15. | Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu. |
16. | Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri. |
17. | Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi. |
18. | Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji. |
19. | Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. |
20. | Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli. |
← Genesis (33/50) → |