Genesis (32/50)  

1. Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye.
2. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu.
3. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu.
4. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa,
5. nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako.
6. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.
7. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili.
8. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka.
9. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Bwana, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema;
10. mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili.
11. Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana.
12. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.
13. Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye;
14. mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini;
15. ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi.
16. Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi.
17. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako?
18. Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu.
19. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta.
20. Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu.
21. Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini.
22. Akaondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki.
23. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo.
24. Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri.
25. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.
26. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki.
27. Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo.
28. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.
29. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.
30. Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka.
31. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake.
32. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.

  Genesis (32/50)