← Genesis (30/50) → |
1. | Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. |
2. | Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? |
3. | Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae juu ya magoti yangu, nami nipate uzao kwa yeye. |
4. | Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. |
5. | Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. |
6. | Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. |
7. | Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. |
8. | Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na ndugu yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. |
9. | Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. |
10. | Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. |
11. | Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. |
12. | Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. |
13. | Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri. |
14. | Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja kondeni, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao. |
15. | Naye akamwambia, Je! Ni jambo dogo kuninyang'anya mume wangu; hata wataka kuzitwaa tunguja za mwanangu pia? Raheli akamwambia, Kwa hiyo atalala kwako usiku huu kwa tunguja za mwanao. |
16. | Yakobo akaja kutoka kondeni jioni, Lea akatoka kumlaki, akasema, Lazima uje kwangu, kwa sababu nimekuajiri, kwa tunguja za mwanangu; akalala kwake usiku ule. |
17. | Mungu akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano. |
18. | Lea akasema, Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nimempa mume wangu mjakazi wangu. Akamwita jina lake Isakari. |
19. | Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita. |
20. | Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni. |
21. | Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina. |
22. | Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo. |
23. | Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu. |
24. | Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Bwana aniongeze mwana mwingine. |
25. | Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu. |
26. | Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia. |
27. | Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako. |
28. | Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa. |
29. | Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu. |
30. | Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, Bwana akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe? |
31. | Akamwuliza, Nikupe nini? Yakobo akasema, Usinipe kitu; ukinifanyia neno hili, nitalisha wanyama wako tena na kuwalinda. |
32. | Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu. |
33. | Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa. |
34. | Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo. |
35. | Basi akatoa siku ile mbuzi waume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe. |
36. | Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia. |
37. | Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito. |
38. | Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa. |
39. | Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka. |
40. | Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani. |
41. | Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito, |
42. | lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo. |
43. | Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda. |
← Genesis (30/50) → |