← Genesis (26/50) → |
1. | Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. |
2. | Bwana akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. |
3. | Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. |
4. | Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. |
5. | Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. |
6. | Isaka akakaa katika Gerari. |
7. | Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. |
8. | Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. |
9. | Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. |
10. | Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. |
11. | Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa. |
12. | Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki. |
13. | Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. |
14. | Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. |
15. | Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. |
16. | Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. |
17. | Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. |
18. | Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. |
19. | Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. |
20. | Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. |
21. | Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. |
22. | Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. |
23. | Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. |
24. | Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. |
25. | Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. |
26. | Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. |
27. | Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? |
28. | Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba Bwana alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe |
29. | ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa Bwana. |
30. | Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. |
31. | Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. |
32. | Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. |
33. | Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. |
34. | Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti. |
35. | Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao. |
← Genesis (26/50) → |