← Genesis (25/50) → |
1. | Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. |
2. | Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua. |
3. | Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi. |
4. | Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura. |
5. | Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. |
6. | Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. |
7. | Hizi ndizo siku za miaka ya maisha ya Ibrahimu alizoishi, miaka mia, na sabini na mitano. |
8. | Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. |
9. | Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre. |
10. | Katika lile shamba alilolinunua Ibrahimu kwa wazawa Hethi, huko ndiko alikozikwa Ibrahimu na Sara mkewe. |
11. | Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi. |
12. | Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu. |
13. | Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao. Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu, |
14. | na Mishma, na Duma, na Masa, |
15. | na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema. |
16. | Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao. |
17. | Na hii ndiyo miaka ya maisha ya Ishmaeli, miaka mia na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake. |
18. | Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati ya ndugu zake wote. |
19. | Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. |
20. | Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. |
21. | Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. |
22. | Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana. |
23. | Bwana akamwambia, |
24. | Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. |
25. | Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. |
26. | Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. |
27. | Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. |
28. | Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo. |
29. | Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. |
30. | Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. |
31. | Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. |
32. | Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? |
33. | Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. |
34. | Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza. |
← Genesis (25/50) → |