← Genesis (24/50) → |
1. | Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. |
2. | Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, |
3. | nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; |
4. | bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. |
5. | Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? |
6. | Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. |
7. | Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; |
8. | na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. |
9. | Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. |
10. | Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. |
11. | Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. |
12. | Naye akasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. |
13. | Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, |
14. | basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. |
15. | Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. |
16. | Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. |
17. | Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. |
18. | Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. |
19. | Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. |
20. | Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. |
21. | Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba Bwana ameifanikisha safari yake ama sivyo. |
22. | Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, |
23. | akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? |
24. | Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. |
25. | Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. |
26. | Yule mtu akainama akamsujudu Bwana. |
27. | Akasema, Na atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. Bwana akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu. |
28. | Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. |
29. | Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. |
30. | Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. |
31. | Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na Bwana, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. |
32. | Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. |
33. | Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. |
34. | Akasema, Mimi ni mtumwa wa Ibrahimu, |
35. | na Bwana amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng'ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda. |
36. | Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo. |
37. | Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao. |
38. | Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke. |
39. | Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami. |
40. | Akaniambia, Bwana, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu. |
41. | Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu. |
42. | Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, |
43. | tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, |
44. | naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke Bwana aliyemwekea mwana wa bwana wangu. |
45. | Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe. |
46. | Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao. |
47. | Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake. |
48. | Nikainama, nikamsujudia Bwana, nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. |
49. | Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto. |
50. | Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa Bwana, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. |
51. | Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema Bwana. |
52. | Ikawa mtumishi wa Ibrahimu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za Bwana. |
53. | Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia. |
54. | Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. |
55. | Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende. |
56. | Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi Bwana amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. |
57. | Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. |
58. | Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. |
59. | Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake. |
60. | Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao. |
61. | Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake. |
62. | Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini. |
63. | Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. |
64. | Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. |
65. | Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. |
66. | Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. |
67. | Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake. |
← Genesis (24/50) → |