| ← Genesis (23/50) → |
| 1. | Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara. |
| 2. | Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. |
| 3. | Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena, |
| 4. | Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. |
| 5. | Wazawa wa Hethi wakamjibu Ibrahimu, wakamwambia, |
| 6. | Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako. |
| 7. | Ibrahimu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi. |
| 8. | Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni bin Sohari, |
| 9. | ili kwamba anipe pango ya Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia. |
| 10. | Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Ibrahimu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema, |
| 11. | Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango iliyomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako. |
| 12. | Ibrahimu akainama mbele ya watu wa nchi. |
| 13. | Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu. |
| 14. | Efroni akamjibu Ibrahimu, akamwambia, |
| 15. | Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, n'nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako. |
| 16. | Ibrahimu akakubali maneno ya Efroni. Ibrahimu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara. |
| 17. | Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango iliyokuwamo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa |
| 18. | kuwa mali yake Ibrahimu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake. |
| 19. | Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. |
| 20. | Na lile shamba, na pango iliyomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia. |
| ← Genesis (23/50) → |