| ← Genesis (20/50) → |
| 1. | Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. |
| 2. | Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. |
| 3. | Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. |
| 4. | Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? |
| 5. | Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. |
| 6. | Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. |
| 7. | Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. |
| 8. | Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana. |
| 9. | Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. |
| 10. | Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? |
| 11. | Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. |
| 12. | Naye kweli ni ndugu yangu, binti wa baba yangu ila siye mwana wa mama yangu, ndipo akawa mke wangu. |
| 13. | Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni ndugu yangu. |
| 14. | Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Ibrahimu, akamrudishia Sara mkewe. |
| 15. | Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, kaa upendapo. |
| 16. | Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote. |
| 17. | Ibrahimu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. |
| 18. | Maana Bwana alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu. |
| ← Genesis (20/50) → |