← Genesis (18/50) → |
1. | Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. |
2. | Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, |
3. | akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. |
4. | Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. |
5. | Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. |
6. | Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. |
7. | Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. |
8. | Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. |
9. | Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. |
10. | Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. |
11. | Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. |
12. | Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? |
13. | Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? |
14. | Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. |
15. | Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka. |
16. | Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. |
17. | Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, |
18. | akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? |
19. | Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. |
20. | Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, |
21. | basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. |
22. | Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. |
23. | Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? |
24. | Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? |
25. | Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? |
26. | Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. |
27. | Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. |
28. | Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. |
29. | Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. |
30. | Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. |
31. | Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. |
32. | Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. |
33. | Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake. |
← Genesis (18/50) → |