← Genesis (16/50) → |
1. | Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. |
2. | Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. |
3. | Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. |
4. | Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. |
5. | Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe. |
6. | Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. |
7. | Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. |
8. | Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. |
9. | Malaika wa Bwana akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. |
10. | Malaika wa Bwana akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. |
11. | Malaika wa Bwana akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana Bwana amesikia kilio cha mateso yako. |
12. | Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. |
13. | Akaliita jina la Bwana aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye? |
14. | Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi. |
15. | Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. |
16. | Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli. |
← Genesis (16/50) → |