| ← Genesis (15/50) → |
| 1. | Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. |
| 2. | Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? |
| 3. | Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. |
| 4. | Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. |
| 5. | Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. |
| 6. | Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. |
| 7. | Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. |
| 8. | Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? |
| 9. | Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. |
| 10. | Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. |
| 11. | Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. |
| 12. | Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. |
| 13. | Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. |
| 14. | Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. |
| 15. | Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. |
| 16. | Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado. |
| 17. | Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. |
| 18. | Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, |
| 19. | Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, |
| 20. | na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, |
| 21. | na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi. |
| ← Genesis (15/50) → |