Genesis (1/50)  

1. Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.
2. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.
3. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.
4. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza.
5. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja.
6. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.
7. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.
8. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.
9. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.
10. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
11. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo.
12. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
13. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;
15. tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo.
16. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.
17. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi
18. na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
19. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne.
20. Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.
21. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
22. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi.
23. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano.
24. Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.
25. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
26. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
27. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
28. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.
29. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;
30. na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo.
31. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.

      Genesis (1/50)