← Galatians (6/6) |
1. | Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. |
2. | Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. |
3. | Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. |
4. | Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. |
5. | Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe. |
6. | Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. |
7. | Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. |
8. | Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. |
9. | Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. |
10. | Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. |
11. | Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe! |
12. | Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. |
13. | Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. |
14. | Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. |
15. | Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. |
16. | Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. |
17. | Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. |
18. | Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina. |
← Galatians (6/6) |