| ← Galatians (4/6) → |
| 1. | Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; |
| 2. | bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba. |
| 3. | Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia. |
| 4. | Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, |
| 5. | kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. |
| 6. | Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. |
| 7. | Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. |
| 8. | Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu. |
| 9. | Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? |
| 10. | Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. |
| 11. | Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. |
| 12. | Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lo lote. |
| 13. | Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; |
| 14. | na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. |
| 15. | Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi. |
| 16. | Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli? |
| 17. | Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa njia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku. |
| 18. | Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu. |
| 19. | Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu; |
| 20. | laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu. |
| 21. | Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria? |
| 22. | Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. |
| 23. | Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. |
| 24. | Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. |
| 25. | Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto. |
| 26. | Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi. |
| 27. | Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume. |
| 28. | Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. |
| 29. | Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. |
| 30. | Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. |
| 31. | Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana. |
| ← Galatians (4/6) → |