Galatians (1/6) → |
1. | Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), |
2. | na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; |
3. | Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; |
4. | ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu. |
5. | Utukufu una yeye milele na milele, Amina. |
6. | Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. |
7. | Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. |
8. | Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. |
9. | Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. |
10. | Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. |
11. | Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. |
12. | Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. |
13. | Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. |
14. | Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. |
15. | Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, |
16. | alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; |
17. | wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. |
18. | Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. |
19. | Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. |
20. | Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. |
21. | Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. |
22. | Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; |
23. | ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. |
24. | Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu. |
Galatians (1/6) → |