Ezra (10/10)    

1. Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana.
2. Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili.
3. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.
4. Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.
5. Ndipo Ezra akaondoka, akawaapisha wakuu wa makuhani, na Walawi, na Israeli wote, ya kwamba watafanya kama hayo. Basi wakaapa.
6. Kisha Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu, akaingia katika chumba cha Yehohanani, mwana wa Eliashibu; hata, alipofika huko, hakula mkate, wala hakunywa maji; kwa maana alilia kwa sababu ya kosa lile la watu wa uhamisho.
7. Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu;
8. na ya kwamba mtu awaye yote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho.
9. Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa kenda, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa.
10. Kisha Ezra, kuhani, akasimama, akawaambia, Mmekosa, mmeoa wanawake wageni, kuiongeza hatia ya Israeli.
11. Sasa basi, ungameni mbele za Bwana, Mungu wa baba zenu, mkatende alipendalo; mkajitenge na watu wa nchi, tena na wanawake wageni.
12. Ndipo mkutano wote wakajibu, wakasema, kwa sauti kuu, Kama ulivyosema katika habari yetu, ndivyo vitupasavyo kutenda.
13. Lakini watu hawa ni wengi, tena ni wakati wa mvua nyingi, nasi hatuwezi kusimama nje, tena kazi hii si kazi ya siku moja, wala ya siku mbili; maana tumekosa sana katika jambo hili.
14. Basi maakida wetu na wawekwe kwa ajili ya mkutano wote, na watu wote walio katika miji yetu, waliooa wanawake wageni, na waje nyakati zilizoamriwa, tena pamoja nao na waje wazee wa kila mji, na makadhi wa miji hiyo, hata ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapotuondokea mbali, jambo hili likamalizike.
15. Yonathani, mwana wa Asaheli, na Yazeya, mwana wa Tikwa, hawa peke yao ndio waliosimama kulipinga neno hilo; na Meshulamu, na Shabethai Mlawi, wakawasaidia.
16. Basi wana wa uhamisho wakafanya hivyo. Na Ezra, kuhani, akatengwa, pamoja na baadhi ya wakuu wa mbari za mababa, kwa hesabu ya mbari ya baba zao; na hao wote kwa majina yao. Wakaketi siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, ili kulichunguza jambo hilo.
17. Wakamaliza mambo ya wanaume wote, waliokuwa wameoa wanawake wageni, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.
18. Basi, miongoni mwa makuhani walionekana wengine waliokuwa wameoa wanawake wageni; wa wana wa Yoshua, mwana wa Yosadaki, na nduguze; Maaseya, na Eliezeri, na Yaribu, na Gedalia.
19. Nao wakatoa ahadi ya kwamba wataachana na wake zao; na kwa kuwa walikuwa na hatia, wakatoa kondoo mume kwa hatia yao.
20. Na wa wana wa Imeri; Hanani, na Zebadia.
21. Na wa wana wa Harimu; Maaseya, na Eliya, na Shemaya, na Yehieli, na Uzia.
22. Na wa wana wa Pashuri; Elioenai, na Maaseya, na Ishmaeli, na Nethaneli, na Yozabadi, na Elasa.
23. Na wa Walawi; Yozabadi, na Shimei, na Kelaya (ndiye Kelita), na Pethahia, na Yuda, na Eliezeri.
24. Na wa waimbaji; Eliashibu. Na wa mabawabu; Shalumu, na Telemu, na Uri.
25. Na wa Israeli; wa wana wa Paroshi; Ramia, na Izia, na Malkiya, na Miyamini, na Eleazari, na Malkiya, na Benaya.
26. Na wa wana wa Elamu; Matania, na Zekaria, na Yehieli, na Abdi, na Yeremothi, na Eliya.
27. Na wa wana wa Zatu; Elioenai, na Eliashibu, na Matania, na Yeremothi, na Zabadi, na Aziza.
28. Na wa wana wa Bebai; Yehohanani, na Hanania, na Zakai, na Athlai.
29. Na wa wana wa Bani; Meshulamu, na Maluki, na Adaya, na Yashubu, na Sheali, na Yeremothi.
30. Na wa wana wa Pahath-Moabu; Adna, na Kelali, na Benaya, na Maaseya, na Matania, na Besaleli, na Binui, na Manase.
31. Na wa wana wa Harimu; Eliezeri, na Ishiya, na Malkiya, na Shemaya, na Shimeoni,
32. na Benyamini, na Maluki, na Shemaria.
33. Na wa wana wa Hashumu; Matenai, na Matata, na Zabadi, na Elifeleti, na Yeremai, na Manase, na Shimei.
34. Na wa wana wa Bani; Maadai, na Amramu, na Ueli,
35. na Benaya, na Bedeya, na Keluhi,
36. na Wania, na Meremothi, na Eliashibu,
37. na Matania, na Matenai, na Yaasu.
38. Na wa wana wa Binui; Shimei,
39. na Shelemia, na Nathani, na Adaya,
40. na Maknadebai, na Shashai, na Sharai,
41. na Azareli, na Shelemia, na Shemaria,
42. na Shalumu, na Amaria, na Yusufu.
43. Na wa wana wa Nebo; Yeieli, na Matithia, na Zabadi, na Zebina, na Ido, na Yoeli, na Benaya.
44. Hao wote walikuwa wameoa wanawake wageni; na wake zao wengine walikuwa wamezaa watoto.

  Ezra (10/10)