Ezekiel (8/48)  

1. Ikawa katika mwaka wa sita, mwezi wa sita, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa nikikaa nyumbani mwangu, wazee wa Yuda nao wali wamekaa mbele yangu, mkono wa Bwana MUNGU ukaniangukia huko.
2. Ndipo nikaangalia, na tazama, kana kwamba ni mfano wa moto; tangu mfano wa viuno vyake na chini, moto; na tangu mfano wa viuno vyake na juu, kana kwamba ni mfano wa mwangaza, kama rangi ya kaharabu.
3. Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu.
4. Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika uwanda.
5. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, inua macho yako sasa, uangalie upande wa kaskazini. Basi nikainua macho yangu, nikaangalia upande wa kaskazini, na tazama, upande wa kaskazini wa mlango, ilikuwako sanamu ile ya wivu, mahali pale pa kuingilia.
6. Akaniambia, Mwanadamu, je! Unayaona wanayoyafanya, yaani, haya machukizo makubwa wanayoyafanya nyumba ya Israeli hapa, hata niende zangu mbali na patakatifu pangu? Lakini utaona tena machukizo makubwa mengine.
7. Akanileta hata mlango wa ua; nami nilipoangalia, tazama, pana tundu katika ukuta.
8. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, toboa sasa katika ukuta huu; nami nilipotoboa, tazama, pana mlango.
9. Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa.
10. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote.
11. Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu.
12. Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, Bwana hatuoni; Bwana ameiacha nchi hii.
13. Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda.
14. Ndipo akanileta mpaka mlango wa kuingilia katika nyumba ya Bwana, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi.
15. Akaniambia, Mwanadamu umeyaona haya? Utaona tena machukizo makubwa kuliko hayo.
16. Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya Bwana, na tazama, mlangoni pa hekalu la Bwana, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la Bwana, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki.
17. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani.
18. Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.

  Ezekiel (8/48)