← Ezekiel (7/48) → |
1. | Tena neno la Bwana likanijia, kusema, |
2. | Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU aiambia hivi nchi ya Israeli; Ni mwisho; mwisho umezijia pembe nne za nchi. |
3. | Sasa mwisho huu unakupata, nami nitakuletea hasira yangu, nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. |
4. | Jicho langu halitakuachilia, wala sitaona huruma; bali nitakupatiliza njia zako, na machukizo yako yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
5. | Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, jambo baya la namna ya peke yake; angalia, linakuja. |
6. | Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja. |
7. | Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani. |
8. | Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. |
9. | Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga. |
10. | Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka. |
11. | Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao. |
12. | Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata wote jamii. |
13. | Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu wote jamii; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake. |
14. | Wamepiga tarumbeta, wameweka vitu vyote tayari; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata wote jamii. |
15. | Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla. |
16. | Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake. |
17. | Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji. |
18. | Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote. |
19. | Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya Bwana; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao. |
20. | Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao. |
21. | Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi. |
22. | Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang'anyi wataingia humo na kupatia unajisi. |
23. | Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu. |
24. | Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi. |
25. | Uharibifu unakuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana. |
26. | Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee. |
27. | Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda sawasawa na njia yao; nami nitawahukumu sawasawa na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
← Ezekiel (7/48) → |