Ezekiel (6/48)  

1. Neno la Bwana likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, uelekeze uso wako uitazame milima ya Israeli, ukaitabirie,
3. ukisema, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi milima na vilima, na vijito na mabonde; Tazama, mimi, naam, mimi, nitaleta upanga juu yenu, nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka,
4. Na madhabahu zenu zitakuwa ukiwa, na sanamu zenu za jua zitavunjika; nami nitawatupa wana wenu waliouawa mbele ya vinyago vyenu.
5. Nami nitaiweka mizoga ya wana wa Israeli mbele ya vinyago vyao; nami nitaitawanya mifupa yenu pande zote za madhabahu zenu.
6. Kila mahali mkaapo miji itaharibika, na mahali palipoinuka patakuwa ukiwa; ili madhabahu zenu ziharibiwe, na kufanywa ukiwa, na vinyago vyenu vivunjwe, na kukoma, na sanamu zenu za jua zikatwe, na kuangushwa, na kazi zenu zifutwe kabisa.
7. Na hao waliouawa wataanguka katikati yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
8. Lakini nitasaza mabaki; maana mtakuwa na baadhi ya watu watakaoukimbia upanga kati ya mataifa, mtakapokuwa mmetawanyika katika nchi za watu.
9. Na hao wa kwenu watakaookoka watanikumbuka kati ya mataifa, watakakochukuliwa mateka, jinsi nilivyoiponda mioyo yao ya kikahaba, iliyoniacha, na macho yao, yaendayo kufanya uasherati na vinyago vyao; nao watajichukia nafsi zao machoni pao wenyewe, kwa sababu ya mabaya yao yote, waliyoyatenda kwa machukizo yao yote.
10. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; sikusema bure kama nitawatenda mabaya hayo.
11. Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.
12. Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni; na yeye aliye karibu atakufa kwa upanga; na yeye atakayesalia, na kuhusuriwa katika mji, atakufa kwa njaa, hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu juu yao.
13. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, watu wa kwao waliouawa watakapokuwa kati ya vinyago vyao, pande zote za madhabahu zao, juu ya kila kilima kirefu, juu ya vilele vya milima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, na chini ya kila mwaloni mnene, pale pale walipovifukizia uvumba mzuri vinyago vyao vyote.
14. Nami nitanyosha mkono wangu juu yao, na kuifanya nchi kuwa maganjo, tena ukiwa mbaya kuliko jangwa upande wa Dibla, katika makao yao yote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

  Ezekiel (6/48)