← Ezekiel (47/48) → |
1. | Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. |
2. | Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. |
3. | Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. |
4. | Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. |
5. | Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. |
6. | Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto. |
7. | Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. |
8. | Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari |
9. | Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. |
10. | Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana. |
11. | Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi. |
12. | Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa. |
13. | Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili. |
14. | Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi. |
15. | Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada; |
16. | Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani. |
17. | Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa kaskazini. |
18. | Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya Israeli, utakuwa mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya mashariki. Huu ndio upande wa mashariki. |
19. | Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini, kuelekea kusini. |
20. | Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi. |
21. | Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na kabila za Israeli. |
22. | Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu hali ya ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni mwa wana Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya kabila za Israeli. |
23. | Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika kabila asema Bwana MUNGU. |
← Ezekiel (47/48) → |