Ezekiel (44/48)  

1. Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.
2. Bwana akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa.
3. Na mkuu, yeye ndiye atakayeketi ndani yake ale chakula mbele za Bwana; ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.
4. Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa Bwana uliijaza nyumba ya Bwana; nikaanguka kifudifudi.
5. Bwana akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya Bwana, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu.
6. Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, katika machukizo yenu yote, na iwatoshe,
7. kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote.
8. Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa kawaida zangu, katika patakatifu pangu.
9. Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.
10. Lakini Walawi waliofarakana nami, hapo Waisraeli walipopotea, waliopotea na kuvifuata vinyago vyao, watachukua uovu wao wenyewe.
11. Hata hivyo watakuwa wahudumu katika patakatifu pangu, wakiwa wasimamizi wa malango ya nyumba, wakihudumu humo nyumbani; watawachinjia watu sadaka za kuteketezwa na dhabihu, nao watasimama mbele yao ili kuwahudumia.
12. Kwa sababu waliwahudumia mbele ya vinyago vyao, wakawa kwazo la uovu kwa nyumba ya Israeli; basi nimeuinua mkono wangu juu yao, asema Bwana MUNGU, nao watachukua uovu wao.
13. Wala hawatanikaribia, kunihudumia katika kazi ya ukuhani, wala hawatakaribia vitu vyangu vitakatifu kimojawapo, vitu vilivyo vitakatifu sana; bali watachukua aibu yao, na machukizo yao yote waliyoyatenda.
14. Lakini nitawafanya kuwa walinzi katika ulinzi wa nyumba, kwa huduma yake yote, na kwa yote yatakayotendeka ndani yake.
15. Lakini makuhani Walawi, wana wa Sadoki, waliolinda ulinzi wa patakatifu pangu, hapo wana wa Israeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia ili kunihudumia; nao watasimama mbele zangu, kunitolea mafuta na damu, asema Bwana MUNGU;
16. wataingia patakatifu pangu, nao wataikaribia meza yangu, ili kunihudumia, nao watalinda ulinzi wangu.
17. Itakuwa, hapo watakapoingia kwa malango ya ua wa ndani, watavikwa mavazi ya kitani; wala sufu haitakuwa juu yao, maadamu wanahudumu katika malango ya ua wa ndani, na ndani ya nyumba.
18. Watakuwa na vilemba vya kitani juu ya vichwa vyao, nao watakuwa na suruali za kitani viunoni mwao; hawatajifunga kiunoni kitu cho chote kifanyacho jasho.
19. Nao watakapotoka kuingia ua wa nje, yaani, ua wa nje wa watu, ndipo watakapoyavua mavazi yao waliyovaa katika huduma yao, na kuyaweka katika vile vyumba vitakatifu, nao watavaa mavazi mengine, wasije wakawatakasa watu kwa mavazi yao.
20. Hawatanyoa vichwa vyao, wala hawataacha nywele zao kuwa ndefu sana; watazipunguza nywele za vichwa vyao tu.
21. Wala kuhani awaye yote hatakunywa mvinyo, aingiapo katika ua wa ndani.
22. Wala hawataoa wanawake wajane, wala mwanamke aliyeachwa na mume wake; lakini watatwaa mabikira wa wazao wa nyumba ya Israeli, au mjane aliyefiwa na mumewe kuhani.
23. Nao watawafundisha watu wangu tofauti iliyopo kati ya vitu vitakatifu na vitu vya sikuzote, na kuwafundisha kupambanua kati ya yaliyo machafu na yaliyo safi.
24. Na katika mashindano watasimama ili kuamua; wataamua sawasawa na hukumu zangu; nao watazishika sheria zangu, na amri zangu, katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa; nao watazitakasa sabato zangu.
25. Wala hawatakaribia maiti na kujitia unajisi; ila kwa ajili ya baba, au mama, au mwana, au binti, au ndugu mwanamume, au ndugu mwanamke asiyeolewa bado, waweza kujitia unajisi.
26. Naye akiisha kutakaswa watamhesabia siku saba.
27. Na katika siku atakayoingia ndani ya patakatifu, katika ua wa ndani, ili kuhudumu ndani ya patakatifu, atatoa sadaka yake ya dhambi, asema Bwana MUNGU.
28. Nao watakuwa na urithi; mimi ni urithi wao; wala hamtawapa milki iwayo yote katika Israeli; mimi ni milki yao.
29. Wataila sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia, na kila kitu katika Israeli kilichowekwa wakfu kitakuwa chao.
30. Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi, ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako.
31. Makuhani hawatakula nyamafu, au iliyoraruliwa, ikiwa ya ndege au ya mnyama.

  Ezekiel (44/48)