← Ezekiel (42/48) → |
1. | Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, njia ya kuelekea upande wa kaskazini; akaniingiza katika chumba kilichopakabili mahali palipotengeka, na kilicholikabili jengo upande wa kaskazini; |
2. | kukabili urefu wa dhiraa mia palikuwa na mlango wa kaskazini, na upana wake ni dhiraa hamsini. |
3. | Kukabili zile dhiraa ishirini za ua wa ndani, na kukabili sakafu ya mawe ya ua wa nje, palikuwa na baraza kukabili baraza katika orofa ya tatu. |
4. | Na mbele ya vile vyumba palikuwa na njia, upana wake dhiraa kumi upande wa ndani, njia ya dhiraa mia, na milango yake ilielekea upande wa kaskazini. |
5. | Basi vile vyumba vya juu vilikuwa vifupi zaidi; kwa maana baraza zile zilivipunguza kuliko zilivyovipunguza vya chini na vya katikati. |
6. | Maana vilikuwa vina orofa tatu, wala havikuwa na nguzo kama nguzo za zile nyua; basi kila kilichokuwa cha juu kilikuwa chembamba kuliko cha chini na cha katikati, kutoka chini. |
7. | Na ukuta ule uliokuwa nje, ubavuni mwa vyumba vile, ulioelekea ua wa nje, kuvikabili vyumba vile, urefu wake ni dhiraa hamsini. |
8. | Maana urefu wa vyumba vile, vilivyokuwa katika ua wa nje, ulikuwa dhiraa hamsini; na tazama, mbele ya hekalu, dhiraa mia. |
9. | Na toka chini ya vyumba vile palikuwa na mahali pa kuingilia upande wa mashariki, mtu aviingiavyo toka ua wa nje. |
10. | Tena palikuwa na vyumba katika unene wa ukuta wa ua, kuukabili upande wa mashariki, kupaelekea mahali palipotengeka, na kulielekea jengo. |
11. | Nayo njia iliyokuwa mbele yake, kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake vyumba vile vilivyokuwa upande wa kaskazini, urefu ule ule, na upana ule ule; na mahali pake pa kutokea palikuwa sawasawa na vipimo vyake, na sawasawa na milango yake. |
12. | Na sawasawa na milango ya vyumba, vilivyoelekea upande wa kusini, palikuwa na mlango katika mwisho wa njia ile; yaani, njia iliyoukabili ukuta upande wa mashariki, mtu akiingia. |
13. | Kisha akaniambia, Vyumba vya upande wa kaskazini, na vyumba vya upande wa kusini, ambavyo vyaelekea mahali palipotengeka, ni vyumba vitakatifu; humo makuhani, wamkaribiao Bwana, watakula vitu vilivyo vitakatifu sana; humo wataviweka vitu vilivyo vitakatifu sana, na sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia; kwa maana mahali hapo ni patakatifu. |
14. | Makuhani watakapoingia ndani, hawatatoka mahali patakatifu kwenda hata ua wa nje; lakini wataweka mavazi yao katika mahali wahudumiapo; maana ni matakatifu; nao watavaa mavazi mengine, na kupakaribia mahali palipo mahali pa watu. |
15. | Basi, alipokuwa amekwisha kuipima nyumba ya ndani, akanileta nje, kwa njia ya lango lililokabili upande wa mashariki, akalipima pande zote. |
16. | Akaupima upande wa mashariki kwa mwanzi wa kupimia, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote. |
17. | Akaupima upande wa kaskazini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote. |
18. | Akaupima upande wa kusini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia. |
19. | Akageuka aelekee upande wa magharibi, akapima mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia. |
20. | Alipima pande zake zote nne; lilikuwa na ukuta pande zote, urefu wake mianzi mia tano, na upana wake mianzi mia tano, ili kupatenga mahali palipo patakatifu, na mahali palipo pa watu wote. |
← Ezekiel (42/48) → |