← Ezekiel (41/48) → |
1. | Akanileta mpaka hekaluni, akaipima miimo, upana wake dhiraa sita upande mmoja, na upana wake dhiraa sita upande wa pili, ambao ulikuwa ni upana wa maskani. |
2. | Na upana wa maingilio yake ulikuwa dhiraa kumi; na mbavu za maingilio zilikuwa dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; akaupima urefu wake, dhiraa arobaini, na upana wake, dhiraa ishirini. |
3. | Kisha akaingia ndani, akapima kila mwimo wa maingilio, dhiraa mbili; nayo maingilio, dhiraa sita; na upana wa maingilio dhiraa saba. |
4. | Akaupima urefu wake; dhiraa ishirini, na upana wake, dhiraa ishirini, mbele ya hekalu; akaniambia, Hapa ndipo mahali patakatifu kuliko kila mahali. |
5. | Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote. |
6. | Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba. |
7. | Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati. |
8. | Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita. |
9. | Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba, |
10. | na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote. |
11. | Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote. |
12. | Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini. |
13. | Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia; na mahali pale palipotengeka na jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia; |
14. | tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki, dhiraa mia. |
15. | Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia; na hekalu la ndani, na kumbi za ua; |
16. | na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za orofa zile tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hata madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa); |
17. | na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje, |
18. | kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili; |
19. | basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote. |
20. | Toka chini hata juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi ukuta wa hekalu. |
21. | Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza. |
22. | Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii ndiyo meza iliyo mbele za Bwana. |
23. | Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili. |
24. | Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili. |
25. | Na milango ya hekalu ilifanyiziwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta zilivyofanyiziwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje. |
26. | Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu, katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya boriti zile nene. |
← Ezekiel (41/48) → |