Ezekiel (4/48)  

1. Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu;
2. ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote.
3. Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.
4. Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao.
5. Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli.
6. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia.
7. Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake.
8. Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako.
9. Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula.
10. Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake.
11. Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake.
12. Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu.
13. Bwana akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza.
14. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na hayawani; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu.
15. Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng'ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo.
16. Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa kushangaa;
17. wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.

  Ezekiel (4/48)